Wanawake Uganda
Kundi la wanawake nchini Uganda wamevua nguo, nusu uchi
kulalamikia kitendo cha polisi wa Uganda anayedaiwa kumdhalilisha kingono
mwanasiasa wa upinzani. Kanda ya video imeonyesha polisi akimtomasatomasa
matiti Bi Ingrid Turinawe wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change
(FDC) baadaya kumkamata kuzuia maandamano ya wiki jana.
Naibu kamishina wa polisi Andrew Kaweesa ameomba radhi na kuahidi kufanya
uchunguzi kutokana na tukio hilo. Tangu uchaguzi mkuu mwaka 2011 ambapo rais
Yoweri Museveni alishinda Uganda imeshuhudia maandamano ya upinzani ambapo
wafuasi wengi wameishia celi za polisi.
Tukio hilo lilisababisha kuwe na ghadhabu ya umma ambapo pia lawama
zilitanda kupinga kukamatwa kwa Bi Turinawe ambaye ni kiongozi wa tawi la
wanawake katika chama cha FDC kinachoongozwa na Kizza Besigye.
Mwandishi wa BBC Siraj Kalyango amesema wanawake hao waliandamana hadi kituo
cha polisi wakiwa vifua wazi na kupeperusha mabango yaliokuwa na
maandishi,''utahisi vipi ikiwa sehemu zako nyeti zitafinywa''.Wanawake sita
walikamatwa baada ya kukataa kufunika vifua vyao, lakini wakaachiwa huru bila
masharti yeyote.
No comments:
Post a Comment